na Victor Eliud, Geita
MGOGORO mkubwa umeibuka kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Geita kati ya wataalamu wa halmashauri hiyo na madiwani wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambao wamepitisha maazimio ya kutaka daktari wa mifugo wa wilaya hiyo Thobias Kiputa, awajibishwe kwa kufunga minada ya mifugo kwa mjibu wa sheria.
Kutokana na hali hiyo, wataalamu hao wametishia kususia ofisi za madiwani hao iwapo lengo lao litafanikiwa.
Dk. Kiputa alifunga minada hiyo inayodaiwa kuwa chini ya uzabuni wa baadhi ya madiwani wa CCM, mwanzoni mwa mwezi Mei mwaka huu baada ya kuibuka kwa ugonjwa wa miguu na midomo wilayani Geita na Nyang’hwale.
Baada ya minada hiyo kufungwa na kuathiri kipato cha madiwani hao waliokuwa na zabuni ya kukusanya mapato yanayotokana na uuzaji na ununuzi wa mifugo hiyo, madiwani hao wa CCM wameamua kuvalia njuga sakata hilo kuhakikisha Dk. Kiputa anatimuliwa kwa maslahi yao binafsi bila kujali athari zitakazojitokeza kwa walaji wa nyama iwapo minada hiyo itafunguliwa.
Katika kikao chao cha kujadili hoja ya CAG, kilichofanyika Agosti 16 mwaka huu chini ya Mwenyekiti Christopher Kadeo na kuhudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Magalula Said, madiwani hao walipitisha maazimio ya kutaka daktari huyo awajibishwe sambamba na kutimuliwa kwenye wilaya hiyo kwa walichodai amekurupuka kufunga minada hiyo ili hali wanajua sheria inamruhusu kufanya hivyo.
Mmoja wa wataalamu hao ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, mbali na kushangazwa na madiwani hao kutaka kuchanganya siasa na kazi za kitaalamu, alisema iwapo serikali haitawadhibiti ipo siku yatatokea matatizo makubwa na kusababisha nchi kuingia kwenye matatizo.
Walimtaka waziri mwenye dhamana ya kusimamia mifugo, kuingilia kati mgogoro huo ili haki itendeke kwa madai kuwa serikali katika mkoa huo imeshindwa kuutatua mbali na ofisi zao kuwa na taarifa za ugonjwa huo kwa kukaa kimya ili kulinda masilahi ya CCM, si mtaalamu ambaye yuko pale kutekeleza sheria bila kujali wadhifa wa mhusika.
Hivi karibuni, Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale, Ibrahimu Marwa, aligeuka mbogo na kuzikataa hoja za baadhi ya madiwani wa CCM kwenye wilaya yake za kutaka atumie wadhifa wake kuagiza minada hiyo kufunguliwa sambamba na kumwajibisha daktari huyo kwa kitendo cha kuifunga minada hiyo.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment