Home » » CUF WAMSHITAKI DC KWA RC

CUF WAMSHITAKI DC KWA RC

na Victor Eliud, Geita
CHAMA cha Wananchi (CUF) wilayani Geita, kimemshitaki Mkuu wa Wilaya (DC) hiyo, Omary Manzie, kwa Mkuu wa Mkoa (RC), Said Magalula, kwa madai ya kutawala kibabe, kushindwa kutatua kero za wananchi na kuwabagua kwa itikadi za vyama.
Hatua hiyo imetokana na malalamiko mbalimbali ya wananchi ambayo yamekuwa yakiwasilishwa kwake kwa ajili ya kuyapatia ufumbuzi, lakini baadhi yao huwatimua ofisini mwake kwa madai hana nafasi ya kusikiliza majungu.
Katibu wa CUF wilayani Geita, Sevelin Malugu, aliliambia gazeti hili jana kuwa, mkuu wa wilaya hiyo, aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete hivi karibuni kwa ajili ya kuwatumika wananchi wote, lakini hali hiyo imekuwa kinyume na matarajio yao.
“Mimi namuona DC wangu ni limbukeni wa madaraka…kama nafasi aliyonayo anakuwa hivyo, je, angepewa ukuu wa mkoa ingelikuwaje au angekuwa yeye ndiye Kikwete si angeliweza kutemea mate watu?” alihoji Malugu.
Kutokana na hali hiyo, Malugu amemwandikia barua Mkuu wa Mkoa wa Geita, akimwomba aingilie kati mgogoro wa ardhi dhidi ya wananchi wa Kijiji cha Nyantorontoro “A” na baadhi ya viongozi wa Idara ya Madini wilayani humo ambao wanadaiwa kumilikisha ardhi ya wananchi kinyume cha sheria.
Katika barua hiyo, anadai kuwa mwekezaji aliyemilikishwa ardhi hiyo kinyume na sheria ni Majaliwa Maziku, ambaye anadaiwa kufanya mazungumzo na viongozi wa idara hiyo kisha kupatiwa eneo hilo licha ya wananchi kudai hawajalipwa fidia ya ardhi yao.
Awali eneo hilo lilikuwa likimilikiwa na wananchi na baadaye mwaka 2004 lilichukuliwa na Kampuni ya Kichina ya Sinohidro Coperation Limited, iliyokuwa ikitengeneza barabara kwa kiwango cha lami kutoka wilayani Geita hadi Buzirayombo wilayani Chato.
Kwamba kwa makubaliano baina ya pande mbili, kampuni hiyo ingeitumia ardhi hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu ya mradi huo kisha kuirejesha mikononi mwa wananchi hao.
Katika mradi huo wananchi hao walitakiwa kuhama maeneo hayo ili kuepuka kupata madhara yatokanayo na shughuli za ulipuaji baruti na vumbi kubwa linalotokana na usagaji wa kokoto, ambapo walilipwa fedha kidogo kwa makubaliano ya miaka mitatu huku wengine wakikosa kabisa.
Hata hivyo baada ya mradi huo kuanza kutekelezwa baadhi ya wananchi walijitokeza na kupeleka malalamiko yao kwa mtendaji wa Kijiji cha Nyankumbu kudai kulipwa fidia ya mazao na nyumba zao zilizoharibiwa baada ya milipuko.
Hatua hiyo ilimlazimu mtendaji wa kijiji hicho kumwandikia barua mkuu wa wilaya hiyo, Septemba 11 mwaka 2006 ikimtaarifu juu ya malalamiko ya kuharibiwa mazao kutokana na milipuko hiyo.
Baadaye ofisi ya mkuu wa wilaya iliandika barua Novemba 8 mwaka 2006 kwenda kwa Meneja wa Tanroads Mkoa wa Mwanza juu ya uwepo wa malalamiko hayo.
Aidha, baada ya mradi huo kukamilika mwaka 2007 wananchi walirejea kwenye maeneo yao ya awali na kuendesha maisha yao, lakini katika hali ya kushangaza hivi karibuni walipewa taarifa kupitia ofisi ya madini wilayani humo kuwa, maeneo hayo yamemilikishwa kwa mwekezaji na kutakiwa kuondoka.
Ofisa Madini wa Kanda ya Ziwa, Juma Kharuna, alikiri eneo hilo kugawiwa kwa mwekezaji na kudai kuwa taratibu zote za kisheria zimezingatiwa kwa kuwa lilikaa wazi kwa muda mrefu mpaka hapo alipojitokeza mwekezaji huyo.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Geita Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa