Home » » Walaji wa nyama Geita hatarini kukumbwa na magonjwa

Walaji wa nyama Geita hatarini kukumbwa na magonjwa



Na David Azaria, Geita Yetu

MADHARA makubwa yanaweza kutokea kwa binadamu na mifugo kutokana uuzwaji wa madawa yaliyopitwa na wakati na yaliyochini ya kiwango unaofanywa na wauzaji wa maduka ya madawa ya mifugo katika wilaya na Mkoa Mpya wa Geita kinyume cha kanuni, sheria na taratibu za biashara hiyo.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi kwa takribani miezi mine sasa umebaini kuwa, asilimia 99 ya maduka ya madawa ya mifugo Wilayani hapa yanamilikiwa na kuendeshwa kinyume cha sheria.

Kwa mjibu wa uchunguzi huo ulioshirikisha vyanzo mbalimbali vya habari umebaini wamiliki wa maduka hayo kuwa ni baadhi ya watumishi wa umma, madiwani na wafanyabiashara wakubwa hali inayowapa ugumu wataalamu waliopewa dhamana ya kusimamia shughuli za mifugo kwenye wilaya hiyo kusimamia sheria ipasavyo kwa kuhofia kibarua chao kuota majani iwapo wataamua kufunga maduka hayo.

Pia uchunguzi huo umebaini kuwa,wamiliki wake pamoja na wauzaji wake hawana taaluma yoyote inayohusiana na madawa hayo ya mifugo hali ambayo ni hatari na inaweza kusababisha madhara kwa mifugo wakiwemo binadamu ambao ni watumiaji wa bidhaa itokanayo na mifugo.

Habari zaidi zinasema kuwa wauzaji hao wanauza madawa ya kuchomea sindano, ambayo kisheria yanapaswa kutolewa na daktari wa mifugo ambaye amepewa dhamana hiyo na si mtu mwingine yeyote kama inavyofanyika kwa sasa.

Kama hiyo haitoshi katika maduka hayo wanauza pia chanjo za mifugo ambazo zinahifadhiwa na kusafirishwa katika mazingira yasiyoruhusiwa kitaalamu jambo ambalo iwapo litafumbiwa macho linaweza kusababisha magonjwa ya mifugo kwa kuwa wanaofanya kazi hiyo si wataalamu na pengine kuhatarisha afya za walaji.

Kisheria Daktari wa mifugo anatakiwa kutoa madawa hayo kwa mtaalamu aliyeko chini yake na si mfugaji wala muuzaji anayeruhusiwa kuuza madawa hayo,ingawa hilo kwa wilaya ya Geita linaonekana kukithiri.

Hata hivyo baadhi ya wafugaji waliozungumza na mwandishi wa habari hii kwa nyakati tofauti walidai kuwa mbali na juhudi zinazofanywa na wataalamu wa mifugo Wilayani hapa kuhakikisha chanjo ya mifugo inakuwa endelevu juhudi hizo zinapigwa vita na baadhi ya madiwani wa halmashauri hiyo.

Madiwani hao na viongozi wa serikalini wanaomiliki maduka hayo wamekuwa wakidhoofisha juhudi za zoezi la kuhakiki ubora wa maduka hayo ya madawa ya mifugo na sifa za wauzaji wake ili kuendelea kufanya biashara yao bila kujali madhara kwa jamii.

“Madiwani wetu wanawapiga vita wataalamu wa mifugo kufanya kazi yao ili waendelee kutuuzia madawa kutoka kwenye maduka yao ndiyo maana hawapendi kuona wataalamu wanatuzungukia kwa ajili ya kuchanja mifugo yetu wao” alisema mmoja wa wafugaji katika kijiji cha Bukoli aliyetaka jina lake lisiandikwe.

Kwa upande wake daktari wa mifugo wa Wilaya ya Geita Thobias Kiputa alipohojiwa kuwepo kwa hali hiyo alikiri kuwepo kwa wimbi la watu kumiliki maduka hayo kinyume cha sheria jambo ambalo linampa wakati mgumu katika utendaji wake wa kazi.

Alisema yuko tayari kufukuzwa kazi kwa kutekeleza kazi yake kwa sababu ya kukagua maduka ya madawa ya mifugo yanayomilikiwa na viongozi serikalini.

“Hapa umenikuta ninapanga mkakati wa kuhakikisha ni jinsi gani nitaweza kuidhibiti hali hiyo…si uongo maduka mengine yanamilikiwa na vigogo hapa wilayani,lakini nataka nikuhakikishie kwamba nipo tayari kufukuzwa kazi lakini lazima niwadhibiti..litakalokuwa na liwe” alisema Dk Kiputa.

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Geita Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa