na Victor Eliud, Geita
WAZIRI wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Hawa Ghasia amewalipua madiwani katika halmashauri ya Wilaya ya Geita Mkoani Geita akidai kuwa baadhi yao wanashirikiana na watumishi wa halmashauri hiyo kusuka mitandao ya wizi wa fedha za serikali.
Katika hilo Ghasia aliahidi kulifanyia kazi kwa kutomuonea aibu mtu yeyote atakayebainika kufuja fedha za serikali.
Kuwepo kwa mitandao hiyo kumesababisha halmashauri hiyo kupata hati yenye mashaka kwa zaidi ya mara moja sasa hatua iliyosababisha baadhi ya miradi ya maendeleo kukamilika chini ya kiwango na mingine kutokamilika kabisa licha ya serikali kutoa fedha.
Waziri Ghasia aliyasema hayo juzi wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na jumuia za watumishi wa serikali madiwani, wakuu wa wilaya za mkoa huo pamoja na wakuu wa idara muda mfupi baada ya mkuu wa mkoa wa Geita Magalula Said kumsomea taarifa ya mkoa huo.
Alisema kitendo cha madiwani na baadhi ya watumishi kuunda mitandao ya wizi wa fedha za serikali ni hatari katika taifa kwani hali hiyo imechangia kuzalisha wezi na majambazi wa kuiba mali za umma kinyume cha sheria za utumishi wa umma.
“Madiwani wamechaguliwa na wananchi kuwawakilisha lakini cha ajabu hao hao ndiyo wamekuwa mstari wa mbele kushirikiana na watumishi wa umma kusuka mitandao ya wizi kwenye halmashauri nyingi nchini na hata hapa Geita…ushahidi tunao,” alisema.
“Hali hiyo ndiyo imepelekea hata halmashauri yenu kupata hati zenye mashaka na hata ripoti ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa fedha za serikali (CAG) imewataja madiwani moja kwa moja ndiyo maana sasa badala ya kusonga mbele kimaendeleo tumekuwa tukisuasua.”
Pia aliwatuhumu madiwani hao kuwa wamekuwa wakijimilikisha tenda za ukandarasi wa barabara, na majengo zinazotangazwa na halmashauri ilhali sheria haiwaruhusu viongozi hao kumiliki tenda ya aina yoyote ndani ya halmashauri yao.
Hatua aliyosema imesababisha baadhi ya miradi inayotekelezwa na serikali kwa kushirikisha nguvu za wananchi kukamilika ikiwa chini ya kiwango kinyume na makusudio ya serikali.
“Mimi ni mtu wa vitendo na katika hili sitomuonea mtu..na sintokuwa na aibu kumuwajibisha yeyote atakayebainika kufuja fedha za serikali kinyume na makusudio ya serikali..ni bora mtu kama huyo nimuondoe kwenye wadhifa wake na si kumhamisha kwenye kituo chake cha kazi..tena nitahitaji aitwe mtuhumiwa kwa kumpeleka mahakamani,” alisema Waziri Ghasia.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment