Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Mhandisi Robert Luhumbi
akizungumza na waandishi wa habari leo mkoani humo kuhusu Kampeni
Maalum ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi iliyoanza leo tarehe 9 hadi 13
Aprili, 2018 ikiwa na lengo la kuelimisha, kusikiliza malalamiko,
changamoto pamoja na kupokea maoni mbalimbali kutoka kwa wafanyabiashara
na wananchi wa mkoa huo.
Meneja
wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Geita akizungumza wakati wa
mkutano wa waandishi wa habari mkoani humo kuhusu Kampeni Maalum ya
Huduma na Elimu kwa Mlipakodi iliyoanza leo tarehe 9 hadi 13 Aprili,
2018 ikiwa na lengo la kuelimisha, kusikiliza malalamiko, changamoto
pamoja na kupokea maoni mbalimbali kutoka kwa wafanyabiashara na
wananchi wa mkoa huo.
Kiongozi
wa timu ya watalaam kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Makao Makuu
Maternus Mallya akizungumza wakati wa mkutano wa waandishi wa habari
mkoani Geita kuhusu Kampeni Maalum ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi
iliyoanza leo tarehe 9 hadi 13 Aprili, 2018 ikiwa na lengo la
kuelimisha, kusikiliza malalamiko, changamoto pamoja na kupokea maoni
mbalimbali kutoka kwa wafanyabiashara na wananchi wa mkoa huo. (PICHA NA
BENEDICT LIWENGA).
Na Veronica Kazimoto
Geita
9 Aprili, 2018
Wito umetolewa kwa wafanyabiashara na
wananchi wa Mkoa wa Geita kujitokeza kwa wingi katika Kampeni Maalum ya
Huduma na Elimu kwa Mlipakodi kwa ajili ya kuwasilisha
malalamiko, changamoto, maoni pamoja na kupata elimu ya masuala ya kodi
na ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwa ujumla.
Akizungumza na waandishi wa habari leo mkoani Geita, Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Mhandisi Robert Luhumbi
amesema kuwa, wafanyabishara na wananchi watumie fursa ya kampeni hii
itakayomalizika tarehe 13 Aprili, 2018 kupata elimu sahihi ya masuala ya
kodi na tozo mbalimbali.
"Nachukua fursa hii kutoa wito kwa wafanyabiashara na wananchi wote wa mkoa huu hususani wale wanaoishi katika maeneo ya Masumbwe, Ushirombo, Rulembela, Katoro, Lunzewe, Namonge, Nyanghw'ale, Bwanga na Muganza
kujitokeza kwa wingi ili waweze kujifunza, kupata huduma na kutoa maoni
yao kwa watalaam wetu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili waweze
kuyatolea ufafanuzi na kuyafanyia kazi," amesema Mhe. Luhumbi.
Nae Meneja wa TRA mkoani hapa, James
Jilala amesema kuwa, lengo kuu la kufanya kampeni hii maalumu ni
kuelimisha, kusikiliza malalamiko, changamoto pamoja na kupokea mrejesho
na maoni mbalimbali kutoka kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla.
"Kampeni hii ni mwendelezo wa Wiki ya
Elimu kwa Mlipakodi iliyofanyika nchi nzima kuanzia tarehe 5 hadi 9
Machi, 2018 katika ngazi ya mkoa. Kutokana na matokeo ya kampeni ile
mkoani hapa, tumeona ni muhimu tuwe na kampeni nyingine maalumu ambayo
inafanyika maeneo mbalimbali katika wilaya zetu tofauti na ile ya kwanza
iliyofanyika Geita mjini tu," amefafanua Jilala.
Kwa upande wake kiongozi wa timu ya
watalaam kutoka TRA Makao Makuu Maternus Mallya ameeleza kuwa, timu yake
imejipanga vizuri na tayari kazi imeanza kufanyika katika vituo vyote
vilivyotengwa kwa ajili ya kampeni hiyo.
"Hapa ninapozungumza, wenzangu wako
kwenye maeneo husika wanaendelea kufanya kazi. Hivyo, kama alivyosema
Mhe. Mkuu wa Mkoa, nami natoa rai kwa wananchi wote mkoani hapa,
kujitokeza kwa wingi ili waweze kukutana na watalaam wetu kwa ajili ya
kupata huduma na elimu ya mlipakodi," amesema Mallya.
Kampeni Maalum ya Huduma na Elimu kwa
Mlipakodi mkoani Geita imeanza leo tarehe 9 hadi 13 Aprili, 2018 ambapo
pamoja na mambo mengine, wafanyabiashara na wananchi watasajiliwa na
kupatiwa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) pamoja na kuelimishwa
kuhusu ulipaji wa Kodi ya Majengo kwa njia ya kieletroniki.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment