POLISI mkoani Geita kwa kushirikiana na wenzao wa Mkoa wa Arusha
wamemtia mbaroni mtuhumiwa wa utekaji watoto akiwa na mtoto mwenye umri
wa miaka miwili katika nyumba ya kulala wageni ya Shitungulu, Katoro
Wilaya na Mkoa Geita aliyekuwa akimshikilia akidai apewe Sh milioni nne.
Samson Peter amekamatwa usiku wa kuamkia jana baada ya timu maalumu
ya Polisi ya askari tisa, watano kutoka Arusha wakiongozwa na Mkaguzi wa
Polisi Amani na wa Geita askari wanne wakiongozwa na Mkaguzi wa Polisi,
James, kuizingira nyumba ya wageni aliyokuwa amejificha mtuhumiwa na
mtoto aliyemteka tangu Septemba Mosi.
Akithibitisha hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli
Mwabulambo alisema mtuhumiwa alikamatwa saa mbili usiku juzi katika
nyumba ya kulala wageni iitwayo Shitungulu katika Mtaa wa California,
Kata ya Katoro wilayani Geita akiwa chumba namba 11 na mtoto huyo
Justine Ombeni (2) aliyemteka, akiwa hai na afya njema.
Kamanda Mwabulambo alisema mtoto huyo alitekwa Septemba Mosi saa nane
mchana wakati akicheza na watoto wengine watatu mbele ya nyumba yao
baada ya mtuhumiwa kufika na kuwagawia jojo watoto wengine watatu na
kisha huyo wa nne kumchukua akiwaambia watoto wenzake akamnunulie juisi
dukani.
Alieleza kuwa baada ya kuwalaghai watoto wengine, aliondoka na mtoto
huyo na kutokomea kusikojulikana hadi wazazi walipotoa taarifa Kituo cha
Polisi Geita na wakati baba anarudi nyumbani kutoka kuripoti Polisi
zikiwa zimepita saa nne baada ya utekaji, alikuta ujumbe wa karatasi
unaoonesha namba ya simu ya mtekaji ukielekeza awasiliane naye kwa simu
hiyo.
Ujumbe huo alipatiwa kijana mwenye umri wa miaka 13 wa jirani ambaye
bila kufahamu una lengo gani aliufikisha nyumbani kwa familia na ndipo
ufuatiliaji ulipoanza wa mtoto kwa kuwasiliana kupitia simu hiyo ambayo
katika mawasiliano, mtekaji alitoa masharti ya kutumiwa Sh milioni nne
kupitia mtandao wa M-Pesa.
Wakati mtekaji huyo akitekeleza ukatili huo, tayari wakati huohuo
alikuwa akisakwa mkoani Arusha kwa tuhuma pia za kuteka watoto wanne na
kisha kujipatia Sh 300,000 kwa njia hiyo ya kupitia mtandao wa simu na
kuwaachia watoto wawili kati ya wanne anaodaiwa kuwateka.
Hadi jana watoto wawili kati ya hao wanne hawajulikani waliko. Kwa
mujibu wa taarifa za kipolisi, imedaiwa kuwa baada ya kutenda ukatili
huo mkoani Arusha kati ya Juni na Agosti, mtuhumiwa alitoroka na kurudi
mkoani Geita na kuendeleza ukatili huo hadi alipotiwa mbaroni na timu
hiyo ya askari polisi waliokuwa wakitumia weledi na utaalamu wa
ufuatiliaji mitandao ya simu.
Akisimulia huku akitokwa machozi, mama mzazi wa mtoto aliyetekwa,
Elizabeth Ombeni alisema anaishukuru zaidi serikali na Jeshi la Polisi
kwa kazi nzuri iliyoifanya kwa kurejesha amani na faraja katika familia
hiyo iliyokuwa imetoweka kwa zaidi ya saa 36.
Kwa upande wake, baba mzazi wa mtoto, Ombeni Mshana alisema
ushirikiano wa Polisi katika kutekeleza kazi hiyo uwe ni mfano wa
maadili mema na kujituma kwa dhati katika ufuatiliaji na kupambana na
uhalifu akiwashukuru polisi mikoa ya Geita na Arusha kwa kufanikisha
uokozi huo.
Alisema baada ya kupewa vitisho kupitia ujumbe wa simu kutoka kwa
mtuhumiwa ukimuonya kuwa akithubutu kuripoti au kushirikiana na polisi
kumsaka atamkata mikono na miguu mtoto wake, ulimshtua sana na alikuwa
ameamua kutuma kiasi cha fedha kilichoombwa na mtuhumiwa kwa simu.
Hata hivyo, alisema polisi walimzuia na kumtia moyo asitume fedha, na
hadi mtuhumiwa anakamatwa alikuwa hajampatia fedha kiasi chochote.
Alipotakiwa kuzungumzia tuhuma hizo, Samson Peter amekiri kuhusika na
kuwa amekuwa akisukumwa na tamaa kupata fedha za matumizi kwa maisha ya
anasa baada ya kukatisha masomo akiwa kidato cha tatu na alihitimu elimu
ya msingi katika Shule ya Msingi Kilimani katika Kata ya Katoro.
Akizungumza na wanahabari baada ya kukamatwa, Peter amekiri kumteka
mtoto Justine ili ajipatie fedha jaribio alilokiri kugonga mwamba na
kuwa kati miezi miwili iliyopita, akiwa jijini Arusha pia aliteka watoto
wanne akiwemo msichana mmoja na kupata Sh 300,000 kabla ya kurudi
mkoani Geita.
Hata hivyo, baada ya wazazi wa watoto wengine wawili kushindwa
kumpatia fedha kupitia mtandao, aliwatelekeza na kuondoka huku wengine
wawili akiwarudisha maeneo aliokuwa amewateka ili warudi kwa wazazi wao
kwa kuwaachia huru baada ya kumpatia fedha hizo kupitia mtandao wa simu.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment