Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
NI kama sinema vile iliyochezwa na majambazi mawili katika mji wa Geita.
Majambazi hayo, juzi yaliuteka mji wa Geita kwa takribani dakika 15
kwa mtutu wa bunduki na kupora fedha huku wakala mkuu wa kutoa huduma za
fedha kupitia mitandao ya simu za mkononi na wakala wa huduma ya CRDB,
Gosbert Walwa, akiuawa kwa kupigwa risasi dukani kwake.
Tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 11 jioni mjini hapa na kuibua
taharuki kubwa kwa wananchi kukimbia kunusuru maisha yao, huku baadhi
ya wafanyabiashara wakifunga maduka kuhofia risasi zilizokuwa
zikivurumishwa muda huo.
Majambazi hayo yalipora fedha kwenye ofisi ya Kampuni ya Blue Coast
Investment Ltd na kwenye ofisi ya wakala wa usambazaji wa bia mjini
Geita, Ignas Athanasi Inyasi.
Baada ya kufanya uporaji huo, majambazi hayo yaliondoka na kufyatua
risasi barabarani na kulishambulia gari moja lililokuwa barabarani
kabla ya kuingia dukani kwa wakala mkuu wa kutoa huduma za fedha kwa
mitandao ya simu, Walwa, ambaye aliuawa nje ya duka lake.
Mmoja wa walioshuhudia tukio hilo, alisema watu hao waliingia ndani
ya duka la Walwa na wakati wanatoka, walikutana naye mlangoni na
kumpiga risasi iliyompata tumboni na kuanguka kisha kupoteza maisha
hapo hapo.
“Hao watu walifika wakaegesha pikipiki yao nje, walikuwa wamevalia
makoti meusi na kichwani walivaa kofia ngumu (Helmet), baada ya kumpiga
Walwa (Wakala), walichukua pikipiki yao wakapiga risasi moja hewani,”
alisikika mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo.
Shuhuda mwingine alisema tukio hilo limetokea umbali wa mita kama 50
kutoka zilipo ofisi za benki za NBC, NMB na Posta, zinazolindwa na
askari polisi ambao walikuwa wakishuhudia sinema nzima ya tukio hilo
bila kutoa msaada.
Mbali na kusababisha mauaji hayo, majambazi hayo yalimjeruhi kwa
risasi Alex James (29), dereva wa Kampuni ya Dolfin raia wa Marekani na
Albert Gasia (25) aliyekuwa kwenye gari alilokuwa akiliendesha James.
Muda mfupi baada ya tukio hilo, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Geita, Busee
Bwire, alifika eneo hilo kwa gari lake akiwa na askari zaidi ya
watano, lakini majambazi hayo yalishatawanyika.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Prudensia Protas,
alithibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kuongeza kwamba polisi wameanza
msako na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment