Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
INJINIA wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Hamis Chande,
amenusurika kupigwa na wananchi wa Kijiji cha Bugulula, wilayani Geita
baada ya kwenda kuangalia msingi wa jengo la Mama na Mtoto linalodaiwa
kujengwa chini ya kiwango.
Tukio hilo limetokea jana, wakati injinia huyo alipofika kijijini
hapo akiwa na mafundi na vifaa kama saruji na nondo kwa ajili ya
kuendelea na ujenzi wa msingi huo ambao ni mbovu, huku wananchi wakitaka
ubomolewe wote na uanze upya bila kujali fedha za kurudia watazipata
wapi.
Wananchi walipomuona injinia huyo walikwenda eneo hilo, walipiga yowe
wakitaka wananchi wakusanyike wapewe majibu ya kutosha kuhusu hatma ya
msingi huo, lakini injinia huyo alikosa majibu, hali iliyosababisha
wananchi waanze kumzonga wakitaka kumpiga wakidai naye ni wale
wanaokula fedha za wananchi kwa kujinufaisha wao wenyewe.
Wakizumgumza kwa nyakati tofauti, wananchi hao walisema wao hawataki
kurekebishwa kwa msingi, bali wanataka ubomolewe na urudiwe kujengwa
upya kwani sh milioni 36 ni pesa nyingi ambazo wanadai zimejenga
msingi huo.
Wakati vurugu hizo zikiendelea, walifika polisi kutoka Kituo Kikuu
cha Wilaya ya Geita wakiwa katika gari PT 1166 na kumuamuru injinia
kuondoka eneo hilo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Ali Kidwaka,
alipoulizwa kwanini amemtuma injinia wake kwenda na mafundi wakati
aliyetakiwa kwenda ni mkandarasi, alikana kumtuma injinia huyo na
mafundi wala kuzungumza chochote, bali alimtuma akakague na kurudisha
majibu.
“Nashaanga kusikia kaenda na mafundi, lakini mimi kama mkurugenzi nasema msingi huo utabomolewa na kujengwa upya,” alisema.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment