Home »
» Barabara ya Masumbwe- Mbogwe yapandishwa hadhi
Barabara ya Masumbwe- Mbogwe yapandishwa hadhi
|
|
WIZARA ya Ujenzi imeipandisha daraja barabara inayounganisha
maeneo ya Masumbwe na Makao Makuu ya Wilaya ya Mbogwe, mkoani Geita
kuwa na hadhi ya mkoa.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jijini Dar es Salaam jana
na kusainiwa na Msemaji wa Wizara ya Ujenzi, Martin Ntemo, ilieleza
awali barabara hiyo ilikuwa ikihudumiwa na wilaya, lakini ikipatiwa
matengenezo ambayo hayakukidhi ongezeko la magari yanayotumia barabara
hiyo kwa sasa.
Alisema Rais Jakaya Kikwete akiwa njiani kutokea mji wa Masumbwe
kupitia makao makuu ya wilaya mpya ya Mbogwe kabla ya kuingia Geita
alisimamishwa mara kadhaa na wananchi wanaoishi katika vijiji inakopita
barabara hiyo ambao walitumia fursa hiyo kuwasilisha kero zao hususan
suala ya barabara hiyo kutokidhi mahitaji.
Ntemo alisema akijibu maombi ya wananchi hao, mbele ya rais, Waziri
wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, alimweleza rais kuwa barabara hiyo
inayolalamikiwa ilikuwa chini ya usimamizi wa wilaya.
Hata hivyo, kwa kuzingatia umuhimu wa barabara hiyo na uchanga wa
wilaya hiyo mpya, alikipokea kilio cha wananchi hao na kukubali
barabara hiyo ipandishwe daraja na kuwa ya mkoa.
“Nitatumia mamlaka niliyopewa chini ya Sheria ya Mfuko wa Barabara
Namba 13 ya mwaka 2007 kuipandisha barabara hii ambayo inaanzia
Masumbwe kupitia Mbogwe, Nyikanga hadi Butengo Lumasa yenye urefu wa
kilometa 81 kwamba itakuwa ya mkoa na hivyo kuwa chini ya usimamizi wa
Tanroads,” alisema Waziri Magufuli.
Katika hatua nyingine, Magufuli alibainisha katika mipango ya mwaka
ujao wa fedha wa 2014/2015, wizara yake itaanza kufanya upembuzi
yakinifu na usanifu wa kina wa barabara inayotokea mji wa Katoro hadi
Ushirombo yenye urefu wa kilometa 56 ili kuijenga kwa kiwango cha lami.
Chanzo;Tanzania Daima
|
|
0 comments:
Post a Comment