KIKOSI dhidi ya
ujangili kanda ya Mwanza kwa kushirikiana na polisi wa vituo vya Nyamboge na
Nzera wilayani Geita wamewakamata wakulima 50 waliokuwa wamewateka wafugaji
sita wa ng'ombe kwa lengo la kuwaua.
Tukio hilo limetokea
juzi majira ya asubuhi kufuatia kuibuka kwa vurugu kati ya wakulima na wafugaji
kugombania maeneo kwenye hifadhi ya Msitu wa Ruande wilayani Geita.
Wakulima hao wakiwa
na silaha za jadi kama mapanga,fimbo,visu na shoka wamekamatwa baada kukutwa
wakiwa wamewazingira wafugaji hao wakitaka kuwaua kwa kuwachinja shingo.
Hatua hiyo inatokana
na wakulima kuwatuhumu wafugaji kwamba wamekuwa wakiwachongea serikalini
wafukuzwe kwenye hifadhi hiyo ili wasiendelee na kilimo.
Kiongozi wa kikosi
hicho cha kuthibiti ujangili,Samweli Mwita ambaye ni ofisa wanyama pori wilaya
ya Nyang'hwale mkoani Geita amesema awali walipata taarifa kutoka kwa wasamalia
wema kwamba kuna wafugaji wametekwa na kundi kubwa la wakulima wanataka kuuawa.
Amesema kikosi hicho
ambacho kilikuwa kinaendelea na doria ya kuwasaka fisi kililazimika kwenda eneo
la tukio kisha kufyatua risasi hewani kuwathibiti wakulima ambao walikuwa
wamewazingira wafugaji wasitawanyike,hatua iliyofanikisha kuwatia nguvuni watu
hao.
Kikosi
hicho kipo katika vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo kikiendelea na doria ya
kuwasaka fisi ambao wamekuwa tishio kwa maisha ya watu hasa watoto baada ya
kutapakaa kwenye makazi ya watu kutokana na uharibifu wa mazingira ndani ya
hifadhi hiyo.
0 comments:
Post a Comment