RAIS MHE. DKT. SAMIA SULUHU HASSAN AKABIDHI TUZO KWA NSSF YA USIMAMIZI NA URATIBU WA HIFADHI YA JAMII KWA SEKTA BINAFSI NCHINI

Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeshinda tuzo ya Usimamizi na Uratibu wa Hifadhi ya Jamii kwa Sekta Binafsi  nchini, wakati wa kilele cha Maonesho ya Saba ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yaliyofanyika kwenye uwanja wa EPZ Bombambili, mkoani Geita. Tuzo hiyo imetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kupokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba wakati wa ufungaji wa maonesho hayo.

Aidha, NSSF imeshinda tuzo ya mshindi wa kwanza katika kundi la Hifadhi ya Jamii na Huduma za Bima zilizotolewa Oktoba 12, 2024 na Mhe. Anthony Mavunde, Waziri wa Madini, wakati wa maonesho hayo.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo, Bw. Mshomba amesema utoaji wa huduma kidijitali umekuwa nyenzo muhimu katika kuhakikisha huduma za NSSF zinawafikia wanachama popote walipo, ikiwemo kufungua madai ya kuomba mafao mbalimbali.

Bw. Mshomba amewataka waajiri wa sekta binafsi kuhakikisha wanasajili wafanyakazi wao NSSF pamoja na kuwasilisha michango kwa wakati, kwani hilo ni takwa la sheria na vilevile kuwezesha Mfuko kuendelea kukua na kutoa huduma bora.

Aidha, Bw. Mshomba ametoa rai kwa watu waliojiajiri wenyewe katika sekta isiyo rasmi wakiwemo wachimbaji wadogo wa madini, mama lishe, baba lishe, boda boda, wavuvi, wakulima, wafugaji na wajasiriamali mbalimbali kujiunga na kuchangia NSSF kwa  sababu ndiyo njia sahihi ya kupunguza umasikini wa kipato na kujikinga dhidi ya majanga mbalimbali.

Naye, Bw. Omary Mziya, Mkurugenzi wa Uendeshaji, amesema Mfuko utaendelea kutoa huduma bora kwa wanachama kupitia mifumo ya TEHAMA ambapo hivi sasa wanachama wanaweza kufungua madai yao kwa njia ya kidijitali bila ya kulazimika kufika katika ofisi za NSSF.

Kwa upande wake, Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa NSSF, Bi. Lulu Mengele amesema kupitia maonesho hayo Mfuko ulifikisha elimu ya hifadhi ya jamii kwa makundi mbalimbali yakiwemo ya wachimbaji wadogo wa madini pamoja na wajasiriamali zaidi 1500 Wilayani Bukombe. "Maonesho ya madini yalikuwa fursa kwa NSSF kufikisha elimu ya hifadhi ya jamii, kuandikisha wanachama wapya kutoka sekta isiyo rasmi, tutoa elimu kuhusu huduma za kidijitali pamoja na fursa za nyumba na viwanja," amesema Bi. Lulu.

Awali, Meneja wa NSSF Mkoa wa Geita, Bi. Winniel Lusingu amesema katika mwaka wa fedha 2024/25, Ofisi ya Mkoa huo imeweka lengo la kukisanya shilingi bilioni 104 na kuwa mwaka wa fedha uliomalizika walikusanya shilingi bilioni 64. Ameshukuru ushirikiano mkubwa wanaopata kutoka kwa uomgozi wa Mkoa huo, Waajiri, Menejimenti na Wafanyakazi wote wa NSSF.


DC MASALLA ASHAURI MAONESHO YA NANENANE YAVUTIE ENEO LA MAZIWA MAKUU

Waandaaji wa maonesho ya Nanenane mikoa ya Kanda ya Ziwa Magharibi Mwanza,Geita na Kagera wameshauriwa kuzidi kuipa hamasha maonesho hayo na kuzifikia nchi zote za maziwa makuu kutokana na Mkoa wa Mwanza kuwa eneo la kimkakati.

Rai hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe.Hassan Masalla alipotembelea baadhi ya mabanda na kujionea na kupata taarifa mbalimbali kutoka kwa washiriki na kuhimiza fursa ya Mwanza kuwa eneo la kimkakati itumike vizuri kuyapa wigo maonesho hayo.

"Mwanza siku chache zijazo itazidi kuimarika hasa katika eneo la usafiri kuanzia wa anga,reli na barabara hivyo ni wakati mwafaka kwa waandaaji kuja na ubunifu wenye sura ya kimataifa utakao leta tija ya kiuchumi.

Amesema ukanda huu wa nchi za maziwa makuu umejaa wakulima na wafugaji,na makundi mengine na katika maonesho haya kuna utoaji wa elimu ya kitaalamu namna ya kupata tija hata ukiwa na mifugo michache au kuvuna mazao bora kwa muda mfupi bila kitegemea mvua.

Aidha Mkuu huyo wa Wilaya amewataka Taasisi mbalimbali zinazotoa huduma za Utafiti wa kilimo kwa ujumla ziongeze huduma hizo kwa wakulima wote nchini kutokana na sekta hiyo kuingiza fedha nyingi hivi sasa.

Viongozi mbalimbali wanaendelea kuyatembelea maonesho hayo yatakayo fikia tamati Agosti 8 mwaka huu.

Kauli mbiu ya maonesho hayo ni”chagua viongozi bora wa Serikali za mitaa kwa maendeleo endelevu ya kilimo,mifugo na uvuvi.”

 


RAS GEITA AYAZINDUA RASMI MAONESHO YA NANENANE KANDA YA ZIWA MAGHARIBI.

Maonesho ya Nanenane 2024 Kanda ya Ziwa Magharibi yamezinduliwa rasmi leo Agosti 3,2024 kwenye viwanja vya Nyamhongolo huku yakionesha kuzidi kupata hamasa kutoka kwa wananchi.

Akifungua maonesho hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Geita,Katibu Tawala wa mkoa huo Mohamed Gombati amesema Jukwaa hilo liendelee kuwa somo kwa makundi mbalimbali yanayolengwa na maonesho hayo.

Akiwa na mwenyeji wake Katibu Tawala wa mkoa wa Mwanza Bw.Balandya Elikana,Gombati amatembelea mabanda mbalimbali na kujionea huduma zitolewazo na Taasisi,Halmashauri na makundi mbalimbali.

"Serikali ya Rais Samia ni kutaka Taifa lijitosheleze kwa chakula,uwekezaji katika kilimo na maendeleo ya viwanda, nimeona fursa hizo kutokea hapa Nanenane,"amesisitiza Gombati

Akitoa taarifa ya maonesho hayo Bw.Balandya amebainisha yamekuwa na tija kwa wajasiriamali kutokana na kupata elimu ya utaalamu namna ya kuendesha shughuli zao.

"Eneo letu idadi kubwa ni wafugaji na wavuvi,Serikali inaendelea kuwekeza katika sekta hii hivyo wakulima wanafaidika kwa kufanya shughuli zao kwa tija",Balandya.

Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji Emil Kasagara amebainisha maonesho ya mwaka huu hadi siku ya jana walikuwa na washiriki zaidi ya 5,000 wakitoa huduma mbalimbali.

Maonesho hayo yatafikia kilele Agosti 8 mwaka huu na mgeni rasmi atakuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Said Mtanda

 

VICTORIOUS CENTRE CENTER OF EXCELLENCY WAWEKA MIKAKATI KUWASAIDIA WENYE USONJI


Na Mwandishi Wetu

KITUO cha Victorious Centre of Excellency nchini Tanzania kimesisitiza dhamira yake ya kujitolea katika kutoa matibabu ya uhuishaji na elimu kwa jamii kuhusu mahitaji maalumu kwa watoto wenye hali ya usonji hapa nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Victorious Centre of Excellency, Sarah Laiser-Sumaye ameelezea dhamira ya kituo hicho jijini Dar es Salaam hivi karibuni kwenye Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela yaliyoratibiwa na Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na Ubalozi wa Afrika Kusini nchini na kituo cha Victorious Centre of Excellence.

Kupitia maadhimisho hayo wadau hao walifanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo upandaji miti, kutoa misaada mbalimbali, kupaka rangi kuta na kusaidia kazi za jikoni kwenye kituo hicho, ikiashiria juhudi zao za pamoja katika kuimarisha maisha ya watoto wenye mahitaji maalumu.

Akizungumza kwenye tukio hilo, Sarah Laiser-Sumaye alisema ongezeko la kesi za hali ya usonji nchini Tanzania na nchi za Afrika kwa ujumla ni jambo la kuchukua hatua mapema, huku utafiti wa hivi karibuni kutoka kituo cha Kudhibiti Magonjwa (CDC) cha nchini Marekani ukibainisha kuwa mtoto mmoja  kati ya watoto 36 wanakabiliwa na changamoto ya hali ya Usonji.

"Watoto wenye hali ya Usonji hukumbana na changamoto katika mawasiliano, kushindwa kutamka maneno vizuri, hukabiliwa na ugumu katika kupokea mafunzo ya kielimu na mara nyingi huonyesha tabia za ukorofi kupindukia," Sarah Laiser-Sumaye alieleza.

 "Changamoto hizi huongezeka zaidi kutokana na uelewa hafifu na imani za kiutamaduni zinazohusiana na changamoto ya Usonji katika ukanda wa Africa,’’.

Hata hivyo, alibainisha kuwa Kituo cha Victorious Centre of Excellency na Victorious Academy vimeibuka kama alama ya matumaini na usaidizi kwa watoto wenye changamoto hiyo na familia zao. 

Kupitia matibabu yao ya uhuishaji na elimu ya mahitaji maalumu, vituo hivyo vinapambana kuleta tofauti inayokusudiwa katika maisha ya watoto hao wenye mahitaji maalumu pamoja na familia zao.

Kituo hicho kinatoa huduma mbalimbali za tiba ya urekebishaji (rehabilitation therapies) na shughuli za ziada kwa watoto wenye hali ya usonji nchini Tanzania kwa lengo la kuwajumuisha katika jamii kupitia juhudi makini za kujengea uelewa wa kijamii.

Katika kuthibitisha uzito na umuhimu wake, tukio hilo lilipambwa na uwepo wa wadau muhimu kutoka taasisi hizo akiwemo Balozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania, Noluthando Mayende-Malepe, Mkuu wa Ofisi ya Msimamizi Mkazi wa UN, Shabnam Mallick, Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Frederick Sumaye.

Wengine ni  Waziri Mstaafu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula, Balozi wa Umoja wa Comoro na Mkuu wa Msafara wa Kidipromasia, Dk. Ahamada El Badaoui Mohamed Fakih pamoja na Mabalozi wengine kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Congo, Algeria, Namibia, Msumbiji na wengine wengi.
 
Balozi Mayende-Malepe, akizungumza kwenye tukio hilo alionyesha kutambua umuhimu wa kazi zinazofanywa na Kituo cha Victorious Centre of Excellency huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano na taasisi kama hiyo ili kuinua ufahamu na kupanua muelekeo wa fikra, mtazamo na maadili ya Hayati Mandela, ikiwa ni pamoja na mapambano dhidi ya uonevu na kusaidia watu wenye uhitaji.

"Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela ni fursa kwa wananchi duniani kote kwa kutambua nguvu zao binafsi za kubadili dunia kuwa sehemu nzuri na njema ya kuishi.Kupitia ushirikiano na taasisi kama Kituo cha Victorious Centre of Excellency, tunatambua pia tunaweza kuwa sehemu ya kuinua ufahamu na kupanua muelekeo wa maadili na fikra za Mandela ikiwa ni pamoja na mapambano dhidi ya ukatili na kusaidia watu wenye uhitaji maalum," Alisema Balozi Mayende-Malepe

Umoja wa Mataifa pia ulionyesha kuguswa kwake na jitihada za Kituo cha Victorious Centre of Excellency huku ukionyesha kutambua umuhimu wa uongozi wa Nelson Mandela na umuhimu wa kukuza maadili yake na kuhamasisha watu kuwa na mchango chanya kwa jamii.

"Kila kitendo uhesabiwa hata kikiwa kidogo. Iwe ni kuchora ukuta au kusaidia kuandaa chakula, michango yetu leo ni sehemu ya jitihada kubwa ya kimataifa ya kupambana na umaskini na ukosefu wa usawa. Vitendo hivi vya huduma hata kikiwa ni kidogo athari zake chanya huenea nje kwa ukubwa zaidi.’’ Alibainisha Bi. Shabnam Mallick, Mkuu wa Ofisi ya Msimamizi Mkazi wa UN nchini Tanzania.

Hatua ya wadau hao ilikuja huku Kituo cha Victorious Centre of Excellency kikiwa kinaendela kujipambanua kama mdau muhimu sio tu katika kutoa huduma zake, bali pia kuwezesha jamii, kukuza ufahamu na kuunda jamii inayowajibika. 

Kupitia juhudi zake endelevu kituo hicho si tu kinabadilisha maisha ya watoto wenye hali ya usonji, bali pia kinawajuza wengine kufuata nyayo za Hayati Nelson Mandela, kufungamanisha dhana ya ‘Ubuntu’ (Utu) na kutimiza wajibu wake kwa kuzingatia mustakabali bora kwa wote.
Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Frederick Sumaye (wa pili kushoto) akizungumza na washiriki wakiwemo Mabalozi wa mataifa mbalimbali nchini Tanzania, pamoja na wakurugenzi wa mashirika katika maadhimisho ya Kimataifa ya Nelson Mandela yaliyoratibiwa na Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na Ubalozi wa Afrika Kusini hapa nchini na kituo cha Victorious Centre of Excellency. Kupitia maadhimisho hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni, wadau hao walifanya shughuli mbalimbali za kijamii katika kituo hicho ikiwemo upandaji miti, utoaji wa misaada ya kijamii, kupaka rangi kuta na kusaidia kazi za jikoni, ikiashiria juhudi zao za pamoja katika kuimarisha maisha ya watoto wenye mahitaji maalumu nchini. Wanaomsikiliza ni Waanzilishi na Wakurugenzi wa kituo hicho akiwemo Bw Filbert Sumaye (Kushoto) na Bi Sarah Laiser-Sumaye (wa pili kulia) pamoja na Mchungaji Dk. Eliona Kimaro (kulia)
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Victorious Centre of Excellency, Sarah Laiser-Sumaye akizungumza na washiriki wakiwemo Mabalozi wa mataifa mbalimbali nchini Tanzania, pamoja na wakurugenzi wa mashirika katika maadhimisho ya Kimataifa ya Nelson Mandela yaliyoratibiwa na Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na Ubalozi wa Afrika Kusini hapa nchini na kituo cha Victorious Centre of Excellency. Kupitia maadhimisho hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni, wadau hao walifanya shughuli mbalimbali za kijamii katika kituo hicho ikiwemo upandaji miti, utoaji wa misaada ya kijamii, kupaka rangi kuta na kusaidia kazi za jikoni, ikiashiria juhudi zao za pamoja katika kuimarisha maisha ya watoto wenye mahitaji maalumu nchini.

WANAFUNZI NAMNA PEKEE YA KUMLIPA RAIS SAMIA NI KUSOMA KWA BIDII-KATIMBA


Na Angela Msimbira, GEITA

NAIBU WAZIRI Ofisi ya Rais TAMISEMI (Elimu), Mhe. Zainab Katimba ametoa rai kwa wanafunzi wote nchini kuhakikisha wanasoma kwa bidii na kufaulu kwa viwango vya juu ili badae walitumikie taifa.

Mhe.Katimba ametoa rai hiyo alipotembelea shule mpya maalum ya wasichana ya sayansi ya Mkoa wa Geita kwa lengo la kukagua miundombinu iliyojengwa na kujionea maboresho yaliyofanywa na serikali katika ujifunzaji na ufundishaji kwenye sekta ya elimu nchini.

Amesema kuwa dhamira ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha watanzania wanapata elimu iliyobora katika mazingira mazuri hivyo ni wajibu wa wanafunzi kusoma kwa bidii ili kutimiza malengo yao.

“Namna pekee ya kumlipa Dkt, Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha na kujenga miundombinu iliyobora na kuhakikisha mnapata elimu bila ada ni kuhakikisha na ninyi mnasoma kwa bidii, mfaulu vizuri na kupata elimu bora ili baadaye muweze kulitumikia taifa.”

Katimba amesema wanafunzi wanapaswa kutambua kuwa Taifa linawategemea, hivyo amewataka kuhakikisha hawafanyi mchezo wakiwa shuleni bali watumie fursa hiyo kujenga kesho yao.

Akitoa taarifa ya elimu Mkoa wa Geita, Katibu Tawala Mkoa huo, Mohamed Gombati amesema kwa upande wa shule ya sekondari ya wasichana imepokea Sh bilioni 3 katika awamu ya kwanza na Juni mwaka huu zimepokelewa Sh bilioni 1.1 kwa ajili ya kukamilisha baadhi ya majengo na tayari imeshaanza kuchukua wanafunzi.

Amesema kwa mwaka 2021/22 Mkoa wa Geita ilipokea Sh bilioni 17, mwaka 2022/23 zilipokelewa Sh bilioni 31 na kwa mwaka 2023/24 zilipokelewa Sh bilioni 32 bila kujumuisha fedha zinazotolewa kugharamia elimu bila ada.

Amesema kuwa katika fedha za ndani zinazoelekezwa kwenye miradi ya maendeleo za asilimia 60 au 40 kiwango kikubwa kinaelekezwa kwenye sekta ya elimu.

Awali, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya wasichana ya sayansi ya Mkoa wa Geita, Mwamin Kagoma amesema shule hiyo imegharimu Sh bilioni 4 na mpaka sasa wanafunzi 172 kati ya 211 waliopangiwa kujiunga na kidato cha tano wameripoti shuleni.







 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Geita Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa