Home » » WATANZANIA WAMECHOSHWA NA UONGOZI WA WAMBA NGOMA

WATANZANIA WAMECHOSHWA NA UONGOZI WA WAMBA NGOMA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
Wiki iliyopita nilitoa mawazo yangu kuhusu wagombea urais na kuwashauri vijana wajitokeze kwa wingi. Kwa kujenga hoja nilitoa mifano ya viongozi watatu mashuhuri waliokuwa viongozi katika mataifa yao na kuonyesha jinsi walivyofanya harakati za siasa na uongozi wangali bado wabichi.
Nimepata maoni mengi, yapo yaliyounga mkono mawazo yangu na yapo ambayo hayakuunga mkono na kutoa mifano ya viongozi na marais walioingia madarakani wakiwa na umri mkubwa, ambao wameongoza vizuri mataifa yao.
Sina ubishi juu ya hilo, lakini wazo langu lilikuwa na dhamira ya kuwahamasisha vijana wajitokeze kugombea, haikuwa dhamira yangu kuwavunja moyo wazee, wala hakuna sehemu niliyodadavua kwa kusema kuwa wazee hawafai kuwa viongozi, bali nilishauri tu kwamba ingefaa wao wabaki kama washauri.
Mjadala wa umri wa kuongoza ni mpana na kila mtu anayo haki ya kutoa mawazo yake na kuamini anavyoamini. Lakini binafsi, bado naamini kuwa kumpa kijana fursa ya kuongoza siyo jambo baya kwani tumewaona vijana walioongoza na kufanya mambo makubwa tu na ukweli wa fikra mpya, kasi mpya na ari mpya bado unabaki paleple, ingawa siyo lazima kila kijana awe na fikra mpya kwani wapo vijana waliotawaliwa na ukale na uhafidhina.
Ipo dhana inayojitokeza siku hizi kuwa ‘uongozi si majaribio,’ wakati kina Julius Nyerere, Patrice Lumumba wa Kongo, Kwame Nkrumah wa Ghana, Keneth Kaunda wa Zambia, Jomo Kenyatta wa Kenya na wengineo waliposhika hatamu za uongozi, hawakuwa na uzoefu wowote zaidi ya ule wa vitabuni na ule uchungu waliokuwa nao wa kunyonywa, kunyanyaswa na kudhulumiwa.
Hawa walikuwa vijana na waliweza kuyahamisha mataifa yao kutoka hatua moja kwenda nyingine. Kweli walifeli, walikwama na walikosea kwa namna moja ama nyingine katika uongozi wao, lakini yapo pia waliyoyafanya tena kwa ufanisi wa kupigiwa mfano.
Bila shaka ujana na fikra mpya siyo sifa pekee za mtu kuwa kiongozi, ipo sifa moja ambayo imekuwa ikifanikisha zaidi katika masuala ya kukusanya watu, kusikilizwa na kufuatwa; hii ni sifa ya mvuto (Charsma). Kiongozi mzuri ni yule mwenye mvuto, anayependeka. Kiongozi wa namna hii hata akikosea, hadhira huwa iko tayari kumsamehe. Ipo mifano ya viongozi hao, mathalan Mwalimu Nyerere, Nelson Mandela, Martin Luther King, Seif Sharif Hamad kwa kuwataja wachache.
Kadhalika, wapo viongozi waliokuwa na mvuto, lakini kwa sababu moja au nyingine katika mchakato wa uongozi wakapoteza mvuto wao, mathalan, Augustine Mrema, Christopher Mtikila na wengineo. Vilevile wapo viongozi waliochaguliwa kutokana na haiba zao, mathalan Jakaya Kikwete, Barack Obama, Andry Rajolina, Mfalme Mswati wa pili na wengineo.
Wapo marais wanaopendwa na watu wao kutokana na vituko vyao, mathalan Jacob Zuma, huyu kuna wakati alipata kupendwa sana na jamii kubwa ya Afrika Kusini kutokana na kuendekeza mfumodume.
Wakati aliposhiriki ngono na dada anayedaiwa kuwa alikuwa na Virusi Vya Ukimwi (VVU), bila kutumia kinga, Zuma alisema kuwa alipomaliza tu kujamiiana alioga, hivyo haiwezekani kuwa aliambukizwa virusi.
Sifa za rais ni nyingi, kwani hata Benjamin Mkapa aliyekuwa mkali, makini na wakati mwingine mbabe, aliweza kuongoza kwa kiasi chake mpaka hivi leo wapo wadadavuaji wanaoona kuwa alikuwa ni rais mzuri kutokana na misimamo na umakini wake.
Ila ni wazi kuwa Watanzania wanahitaji rais mwenye mawazo mapya, makini, mchapakazi, anayechukia rushwa, ambaye atahakikisha kwamba inapungua kwa asilimia 90 au inatokomezwa kabisa. Watanzania wanahitaji rais atakayelitoa taifa hapa lilipo na kulifikisha katika hatua nyingine ya maendeleo.

Tunataka kiongozi mwenye visheni inayotekelezeka, anayeweza kuyageuza mawazo kuwa vitendo. Tunataka kuiona Tanzania iking’ara kama Singapore, Malaysia, Korea ya Kusini na nchi nyinginezo, ambazo katika miaka ya 60 uchumi wake ulikuwa mdogo, lakini hivi sasa zina uchumi mkubwa na maendeleo ya kuridhisha.
Mara nyingine hizi kelele tunazopiga (za kisiasa) zinasababishwa na kutoridhika na uongozi uliopo. Uongozi wa wamba ngoma, ngozi huvutia kwao. Wanataka viongozi wanaogawa majukumu na kuyafuatilia, viongozi wasioridhika na maneno, viongozi wachapakazi, viongozi wanaoufanya wizi kuwa ni mwiko kwao.
Rais aliye katika taswira ya Watanzania walio wengi ni asiye mbinafsi, atakayelinda masilahi ya watu wa taifa hili, rais asiyeyumbishwa na wabangaizaji, mapapa na manyangumi ya rushwa na ufisadi. Rais atakayelinda mali na dhamana za Watanzania.
Rais mwenye pupa ya maendeleo, rais asiyelala usingizi akikumbuka kuwa mamia kwa maelfu ya Watanzania hawana maji safi na salama, maelfu umeme haujawafikia, hawapati huduma bora za afya na mamilioni ya watoto na vijana hawapati elimu yenye manufaa.
Rais atakayeumwa na njaa inayowakabili Watanzania, atakayetamani mkate anaokula yeye Ikulu wale watu wake wote, pengine rais huyu ni wa kusadikika, lakini Waswahili husema:
“Fikra njema hujenga,” hivyo rais aliye katika fikara za Watanzania ni rais mwenye sifa zote nzuri, lakini kubwa ni kuwa aumwe na shida za Watanzania, awaondoe katika umaskini walio nao, awatoe katika dhuluma zinazowakabili na awafutie ujinga uliotawala vichwani mwao na kuwakinga na adui maradhi.
Hizo ni dhamira tulizokuwa nazo kabla ya uhuru na hadi sasa zitaendelea kuwa ndizo vipaumbele vyetu kama taifa, rais atakayeweza kutimiza hayo, ndiye atakayetufaa, awe kijana, mzee au kikongwe. Rais Robert Mugabe ni kikongwe, lakini bado anaendelea kupendwa na Wazimbabwe walio wengi kwa sababu moja tu kubwa; hajaacha kutoa matumaini kwa wananchi wake iwe kuna jua ama mvua
Chanzo:Mwananchi 

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Geita Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa